The indiginous of Mwanza
Jamii ya Sukuma !
MAANA YA NENO WASUKUMA
Wasukuma ni mkusnyiko wa makundi madogomadogo kutoka maeneo jirani , na
kwamba kundi kubwa zaidi likiwa limetoka Kusini mwa eneo hili la mkoa
wa Mwanza.Jina hili limetokana na neno SUKUMA maana yake wa lugha ya
Kisukuma na Kinyamwezi KASKAZINI, yaani moja wapo wa ya pande nne a dunia
yetu. Wanyamwezi ambao lugha yao inafanana sana na Kisukuma hutuita
sisi tulio Kaskazini mwao "Bhasukuma" yaani watu wa KASKAZINI. Nasi
huwaita "Bhadakama" yaani watu wa KUSINI.Tangu siku zote, wasukuma na wanyamwezi walijulikana kuwa wao ni
"Bhantu" na kutokana na neno hilo kumekuja kujulikana kundi linaloitwa
WABANTU. Kundi hili mara zote limetambulikana kwa lugha wanayozungumza ya
KIBANTU. Hivyo, Wanyamwezi, Wakimbu hadi Wabemba walioko Zambia ni kundi
kubwa la wabantu kufuatia lugha wanazozungumza.
Taarifa zingine kuhusu chimbuko la wasukuma kutoka kwenye mtandao wa
internet kwenye anwani hii.
Kwa mujibu wa simulizi za kihistoria, chifu wa kwana katika eneo la usukuma alikuwa mpwa wa Nkanda akiwa chini ya usimamizi wa baba yake, chifu Muletwa wa Mtemi wa Lushamba ambaye alisafiri mpaka maeneo ya karibu na Kinango na Magaka (kati ya Bujora na Magu) akitokea Nyalukalanga Geita. Katika lugha yake ya asili Nkanda alisema "Lnye Nsukumala aha" yaani "na tupumzike/tuishi hapa" hii inawezekana kuwa ndichi chano cha neno sukuma. Baadaye, kama mzee Nkamba wa kamati ya utafiti Bujora anavyosimulia, Nkanda alikaribishwa na Waruli, wenyeji wa eneo lile ili awe chifu/kiongozi wao. Waliamini kwamba Nkanda alikuwa na dawa inayofanya watu na wanyama wamuogope, vlvile dawa ya kujikinga na mamba mabao mara nyingi waliharibu nyavu ao za uvuvi wa samaki. Alisadikika hata kuwa na uwezo wa kuleta mvua. Nkanda alikataa uteuzi huo kwa sababu desturi ya watu ake Bhalongo na Bhabinza walidai kwamba kiongozi sharti awe mtoto wa binti aliyezaliwa kutoka ukoo a chifu. Nkanda alirejea kijijini kwake ambapo baba yake alimteua Sanga, mtoto wa dada yake nkanda, kuwa kiongozi wa eneo lile ambapo alipumzika kwa mara ya kwanza. Eneo hili bado linajulikana kama Nsukumale (Nsukumala aha) na limeendelea kutoka utemi/utawala mmoja wa kwanza kabisa wa kisukuma hadi temi hamsini na mbili za usukuma siku hizi.
Masimulizi mengine ya hadithi hii kwa mujibu wa Ilembo, pia kutoka Nyalukalanga, aliyekwenda hadi Seke akiwa mwindaji - yeye aliwaalika dada zake wanne (mmoja wao ni Minza) na walikuwa akinadada hao waliokaa kuanzisha temi za Usukuma, Ntuzu na Ng'wagala na watu wengine waliotokea Lukalanga walifuatia baadaye.
Inasemekana Nkanda alimuoa Minza na akawa amirijeshi mkuu wa Ilembo ambapo aliwajibika kuwaunganisha watu wote wa maeneo hayo kama ilivyoelezwa kwenye historia ya vita vya maeneo hayo. Kama ni kweli au si kweli kwamba simulizi hizi mbili zinatoa chimbuko la historia hii basi kwa uhakika zinatoa historia ya utoto wa Nkanda na umuhimu wake katika kuanzisha utawala wa kisukuma. Karibu kila ukoo (luganda) na utemi uliokuwepo kabla au baada ya Nkanda hudai kujihusisha naye hivyo kuonyesha umuhimu wa "Wababhinza na Bhalongo" (ukoo wa wahunzi) unavyohusika katika usukuma.
Kwa kweli simulizi za mwanzo zilizopitiwa na viongozi wa kisukuma na mashujaa wao humhusisha Nkanda na chimbuko la wasukuma na simulizi za pili zimetolewa kwa mtizamo wa Sukuma na Ntuzu.
Iwapo Minza alikuwa mama, dada au mke wa Nkanda, ni wazi kwamba uongozi wa Nkanda uliimarisha jamii na ulisisitiza utamaduni wa Bhabinza katika usukuma. Leo hii salam za jadi za wasukuma ni Iminza - rejeo moja kwa moja la minza, familia yake na jamii ya Bhabinza. Salamu hiyo hujibiwa kwa jina la babu wa mtu aliyejibu na kuonyesha umuhmu wa utiii wa wasukuma kwa mtemi na familia yake. Vile vile husaidia wazazi kuepusha watu wa uhusiao wa karibu wasioane.
UTAWALA
KABLA YA UTAWALA WA Kichifu, jamii ya wasukuma ilikuwa na utawala wa
kiukoo. Ukoo ulisimamia masuala yote ya kiuchui, ardhi, kijamii, ulinzi
na usalama ambapo baba ndiye aliyekuwa kiongozi mkuu wa kaya na mama
alikuwa kitambulisho cha ukoo. Hii ndiyo maana majina yote ya koo za
kisukuma ni majina ya wanawake kama Bhasega, Bhakwimba, Bhashi, Bhagolo,
Bhakimbu, Bhabinza n.k.Utawala wa watemi Usukumani unasadikika kuanza na ujio wa Nyamhindi
(Mhindi) ambaye alikuwa binti mfalme aliyetoroka kwao kuepuka adhabu ya
kifo kutokana na kupata mimba nje ya ndoa. Inaaminika kwamba mama huyu
asili yake ni Uganda/Karagwe kutokana na matumizi ya jina Kabale ambapo
kuna kijiji kiitwacho Kabale huko Uganda, pia Karagwe, Bukoba, Kibondo
na baadhi ya sehemu za Mwanza katika Temi za Buhungukila, Nela na
Bhusumabhu.Inasadikika, Nyampindi alifikia eneo la Mhande (wakati huo ni msitu)
ambalo lilikuwa Buhungukila. Hapo ndipo alipozaliwa Solasi (chukua nchi)
mtemi wa kwanza. Hivyo, inasadikika utawala wa kitemi usukumani
ulianzia hapo. Nyamhindi alizaa mabinti ambao ni Nkwimba,Kabula, Hollo, Gigwa
na Kijiku. Mabinti hawa waligawiwa maeneo ya kwenda kuishi na watoto
wao ambao baadaye walianzisha tawala za kitemi.
Watoto wa Kabula walianzisha Nela, Gigwa na Hollo walianzisha Busumabu,
Kijiku na Nkwimba walianzisha Buhungukila. Watu wa Temi hizi baadaye
walijulikiana kama Bakwimba kutokana na jina la binti mkubwa wa
Nyamhindi.Orodha ya watemi wa Buhungukila
Na Jina la Mtemi Muda wa Utawala Sehemu aliyofia 01 Solasi Mhindi (Nyamhindi) Nyasuma 1555-1581 Mhande 02 Nkobagwambogo Nkwimba 1581-1607 Mhande 03 Nungonhyibamayila/Kijiku 1607-1613 Mhande 04 Masanja I Kijiku 1613-1621 Ng'wampuje 05 Ng'wiza Mholya Kijiku 1621-1634 Busongo 06 Hamu wa ng'wa Kijiku 1634-1650 Ihanga 07 Kumalija wa ng'wa Kijiku 1650-1658 Ihanga 08 Wauzala wa ng'wa Nkwaya 1658-1676 Nhindu 09 Nyanga wa ng'wa Nyandalo 1676-1704 Nkalagwe 10 Matimbya wa ng'wa Nkwimba 1704-1715 Ituja 11 Nchambe wa ng'wa Nkwimba 1715-1731 Ituja 12 Kumalija wa ng'wa Nkwimba 1731-1746 Ituja 13 Balenda wa ng'wa Kubipa 1746-1754 Mhawa 14 Masanja II wa ng'wa Kubipa 1754-1760 Sese 15 Kimoku wa ng'wa Kundi 1760-1784 Lukanga 16 Kwiyenha wa ng'wa Kumba 1784-1812 Lukanga 17 Sengamatindi wa ng'wa Winga 1812-1815 Nyang'hungulu 18 Kasisa wa ng'wa Winga 1815-1820 Nyang'hungulu 19 Mhalule wa ng'wa Kubipa 1820-1827 Nyalugembe 20 Masule wa ng'wa Kubipa 1827-1830 Nyalugembe 21 Masanja III wa ng'wa Kuipa 1830-1836 Nyalugembe 22 Mbuga wa ng'wa Kubipa 1836-1838 Nyalugembe 23 Kabuli wa ng'wa Kubipa 1838-1855 Nyalugembe 24 Kwiyenha wa ng'wa Kwangu 1855-1894 Busongo 25 Muhoja wa ng'wa Kabula 1894- alifukuzwa Busongo Busongo 26 Swiza wa ng'wa Nyasha 1895-1896 alifukuzwa Busongo Busongo 27 Mpuya I wa ng'wa Kwangu Kasadi 1896-1920 Busongo 28 Kwiyukwa wa ng'wa ng'wa Mpuya 1920-1922 Busongo 29 Mpuya II wa Ng'wa Machibya 1931 - 1950 alifukuzwa Busongo 30 Celestini wa Ng'wa Amede 1970 mpaka sasa (2001) Busongo
UCHUMI
Shughuli za kiuchumi kwa jamii ya kisukuma ni kilimo na ufugaji. Hata
hivyo kulikuwa na shughuli kidogo za kiufundi uwindaji na biashara. Kwa
misingi hiyo kila familia ya kisukuma ilijitosheleza kwa mahitaji
kutokana na uzalishaji wake.ARDHI
Wakati wa utawala wa ukoo, ardhi ya ukoo ilikuwa mikononi mwa mkuu wa
ukoo ambaye aliwagawia wanaukoo kwa matumizi. Baada ya kuanza kwa
utawala wa watemi ardhi iliwekwa mikononi mwa Chifu ambaye alimiliki kwa
niaba ya jamii nzima. Ugawaji wa ardhi ulifanywa na wanangwa.Mtu akihama,
anakabidhi ardhi kwa Ng'wanangwa ambaye aliwagawia watu wengine wenye
mahitaji. Baada ya mavuno ya kwanza yule aliyepewa ardhi alifanya sherehe
na kumkaribisha Ng'wanangwa na majirani kwa ajili ya shukrani.KINGA.
Kila mkuu wa kaya alikuwa na jukumu la familia yake dhidi ya maradhi
mbalimbali. Njia kuu ya kinga ilikuwa ni zindiko dhidi ya mabalaa,
maradhi na hata uchawi. Kazi hii ilifanywa na mwenyewe au alitafuta mtaalam
(mganga wa jadi). Zindiko(Lukago) kuu ilikuwa ni kwa ajili ya kuzindika
kaya nzima kwa kuchanja chale (Salago) kwa ajili ya kumzindika mtu mmoja mmoja.Pia kulikuwa na mazindiko kwa ajili ya mifugo,mazao na kinga dhidi ya
wadudu na wanyama waharibifu.Baada ya kuenea kwa dini za kikristo na kiislam kuna watu wachache siku
hizi ambao bado wanaendelea na utaratribu wa mazindiko.MATIBABU
Ilitokea wakati watu aliugua na hata kutokea milipuko ya magonjwa kwa
hiyo ilikuwepo haja ya kuwa na tiba. Magonjwa ya mlipuko yaliyojitokeza
sana ni uti wa mgongo (buhama) na ndui (ndubhi). Magonjwa mengine ambayo
yamekuwa yakishughulikiwa ni kifafa, ukoma (mbiji), matatizo ya uzazi
(bugumba) mshipa wa ngiri na kupooza.Mkuu wa kaya alishughulikia matatizo haya, wakati mwingine alipata
ushauri kutoka kwa majirani na maumivu yakizidi mgonjwa alipelekwa kwa
mganga wa jadi mwenye taaluma ya ugonjwa huo.Waganga wa jadi walipata taaluma yao kwa njia ya mafunzo kwa vitendo.
Mwanafunzi (ng'hemba) alichagua mganga wa kumfundisha (kuhembekwa) na
huko alikwenda kuishi kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi akipata
mafunzo kwa kushiriki katika kwenda kutafuta na kuchimba dawa, kuchanganya
dawa na hatimaye kutibu wagonjwa.Jamii ya kisukuma ilikuwa na waganga wa jadi wa aina mbalimbali:-
waganga wa tiba (bhafumu)
wapiga ramli ambao walibashiri tatizo linalosumbua mtu, hawa walitumia
mtama na minyaa, kuku au ndege (mbalaga).Watabiri wa mvua (bhagemi bha mbula), walitabiri hali ya hewa hasa mvua
kwa ajili ya kilimo. Inasadikika taaluma hii ilitoka kwa Wataturu.Baada ya mwanafunzi kuhitimi alilipa ada ya ya mafunzo ("mhela"), ng'ombe 5 hadi
10 na kuagwa na mwalimu wake (bhabha bhuhemba).Dawa nyingi zilizotumika wakati huo ni za miti shamba. Lakini
walikuwepo waganga wa mifupa waliotibu mgonjwa bila kumgusa (mfano Ng'wana Gege
wa Ndagalu). Wengine walitibu sumu ya nyoka kwa kuloweka nguo aliyokuwa
amevaa mtu aliyeumwa na nyoka kisha kuikamua na mgonjwa wakati huo
hutapika sumu ya nyoka.BURUDANI
Ngoma katika jamii ya kisukuma zilitumika wakati wa kuapisha au
kusimika watemi, kama zana za kazi, wakati wa sherehe, matambiko na kwa
burudani kwa ujumla.Nyakati za kazi hasa kilimo, ngoma za Bugobogobo na Bakomyalume
zilihusika sana. Vikundi hivi wakati wa kilimo vilijihusisha zaidi na kilimo,
kwa kupeana zamu ya kulima kwa kila mwanakikundi. Baada ya msimu wa
kilimo, vikundi hivi vilijihusisha na ngoma za burudani.Nyakati za sherehe za arusi akina mama walikuwa na ngoma yao ya kadandi
au zinzi. Ngoma nyingine zilialikwa kushiriki kulingana na mahitaji ya
mwenye arusi. Kwa sasa ngoma hii haichezwi tena; badala yake kuna
"masalikula" kwa upande wa Busumabu. Ngoma ya wanaume wakati wa sherehe
ilikuwa ni Buswezi. Hawa walivaa mapembe na shanga usoni, hivyo kuficha
nyuso zao. Wao waliomba dua ndoa idumu na iwe na mafanikio hasa katika
kuzaa watoto. Lugha waliyotumia ni ngeni hasa kutokea magharibi (Uganda).Ngoma za burudani zilichezwa hasa wakati wa kiangazi; ngoma hizo ni
pamoja Buyeye/Bucheye (majoka) Bununguli (Nungunungu), Bayege (bugunda) pia
Wigashe (kukaa) ambayo haikuhusisha matumizi ya ngoma, bali tenzi zilizohusu
matukio mbalimbali katika jamii na Beni /Pubha ambayo ni maarufu hadi sasa.Bumanga, hii ni ngoma ya waganga wa jadi kwa ajili ya kupokea wanachama
wapya. Kila mwanafunzi aliyehitimu uganga alipaswa kufanya tambiko ili
aweze kufanya kazi yake ya uganga kwa mafanikio. Ngoma ya bamanga
ilikuwa na madaraja manne;daraja la kwanza Basambe,
la pili Bhufumu, la
tatu Ilungu nala nne Bumanga.
Milango, ngoma hizi zilihusu watemi na mitambiko yao. Zilipigwa wakati
wa kutawazwa mtemi na wakati wa kunyolewa kwake- tukio lililokuwa
likifanyika mara moja kwa mwaka. Wakati wa milango, ngoma zote katika utemi
ule zilialikwa. Tambiko la kunyolewa kwa mtemi lilifanyika ili
kuutakasa mwaka unaofuata uwe wa neema, mvua zinyeshe vizuri, mazao yapatikane
kwa wingi na maradhi mbalimbali kwa watu na mifugo yao yaepushwe. Pia
zoezi la kunyoa mtemi lilisaidia kuweka kumbukumbu za muda au utawala wa
mtemi, kwa sababu kila mwaka liliwekwa jiwe kwa ajili ya kumbukumbu
hiyo kando ya kaburi la mtemi aliyetangulia.Butambi, hii ni sherehe kwa mashujaa. Watu waliofanya matukio makubwa
katika jamii. Matukio haya ni kama yale ya kuua simba, kwenda nyalanja
umasaini na kwenda pwani kisha kurudi salaama. Wakati wa kurudi watu hawa hawakuruhusiwa kupita kwenye mlango ( "mita" ) uleule unaotumiwa na watu wote, ulitengenezwa mlango mwingine na ndipo walipoingilia ;shujaa hutakiwa kuruka zizi(Kubhela Mita)na kuingia nyumbani.Aina nyingine ya mchezo ilikuwa "Nhega" ambao ulichezwa baina ya kijiji
na kijiji na ulihusisha vijana wa kiume tu. Mchezo huu unafanana na
'hockey'. Kijiji kilichoshinda "mechi' kiliichukua "Nhega" na kwenda
kulala nayo kijijini kwao.IBADA
Kabla ya ujio wa dini za kikristu na kiislam jamii ya wasukuma
waliabudu mizimu( "masamva"). Mizimu iliunganisha wale walio hai na waliokufa
(bakulugenji). Jamii ilipopatwa na balaa au maafa ilisadikika kwamba mizimu
imeudhika hivyo ilihitaji kupozwa au kutafuta suluhu kwa njia ya matambiko
(shitambo).Mitambiko mingi uilihusisha wanyama hasa kondoo, mbuzi na pombe ya
mtama. Mitambiko hii ilikuwa katika ngazi mbalimbali; ngazi ya kaya au
familia, ngazi ya ukoo, ngazi ya vikundi maalum na jamii nzima.KUZALIWA MTOTO
Mtoto alipozaliwa hakupewa jia mara moja na wazazi wake. Babu yake
alitaarifiwa na alikuja kumpa jina ambalo litakuwa na maana katika makuzi
yake. Hapa pombe ya mtama iliandaliwa- hii inaweza kufananishwa na
ubatizo labda katika desturi la kikiristo.Mapacha (mabhasa) yalihusisha ngoma ya Babasana ambayo
madhumuni yake yalikuwa kuwatakasa watoto mapacha, familia husika na jamii
kwa ujumla. Mapacha yalihusisha pia watoto waliozaliwa wametanguliza miguu
(kashinje). Watoto waliozaliwa mapacha na wale waliofuatia walipewa
majina maalum;Kulwa na Doto (wa kwanza na wa pili),
Shija (uzao baada ya mapacha),
Muhoja(uzao wa pili baada ya mapacha,
Kamuli (uzao wa tatu baada ya mapachana
Kasanda (Uzao wa nne baada ya mapacha.
MASAMVA (mahugi)-
kila mkuu wa kaya alikuwa na wajibu wa kufanya
mitambiko ya kutuliza mizimu ya wanafamilia yake. Mara nyingi alimwita babu
wa mhusika kuja kumuimarisha (kudimiwa) katika uhusiano wake na mizimu.IHANE-
vijana wa kiume ambao wanaingia katika umri wa kuoa walipaswa
'kuhanwa' yaani kupata mafunzo ya majina ya miti na matumizi yake na
mafunzo mengine.MAZISHI
Mara mtu alipofariki katika jamii ya kisukuma alikunjwa miguu kuja
kifuani kabla ya mazishi. Makundi mbalimbali ya jamii yalikuwa na aina yake
ya mazishi. Aina kuu za mazishi zilikuwa nne. Wanawake, wanaume waganga
na machifu.Mwanaume aliyekuwa na zizi la ng'ombe alizikwa katikati ya
zizi.Wanawake walizikwa kwa kulalia upande wa mkono wao wa kulia
wanaume kulalia upande wa mkono wao wa kushoto..
Waganga walizikwa wakiwa wamekaa kwenye kiti
(nzule) huku wakiwa wameshikishwa mizizi ya dawa. Watemi walizikwa
wakiwa wamekaa kwenye kiti (nzule) wakiwa wameshikishwa mkuki. Baada ya
kaburi kufukiwa liliwekwa jiwe juu yake kama alama ya utambulisho (Ishigo)
kwa kaburi.ELIMU
Elimu ya jadi ilitolewa tangu zama za kale kwa kuzingatia rika, jinsia,
koo, mahitaji na kipindi. Elimu ilitolewa kwa njia ya mapokeo, wazee
kuwasimulia vijana.Kwa wanaume elimu hii ilitolewa hasa wakati wa usiku
wakiota moto (hashikome).Kwa wanawake ilitolewa hasa nyakati za usiku
wakati wa kupika (ha mahiga).Pia elimu ilitolewa kwa njia ya hadithi
kwa vijana wa kiume na wa kike wenye umri mdogo; msimulizi mkuu akiwa
bibi au babu.
(Marehemu Bulunguti Ng'wanamleka Mkuu wa Jamii ya "Bhagalu" Akiwa kwake)
(Nyumba ya mizimu (Masanva) katika jamii ya kisukuma)